Wanaodaiwa kumuua Padri Mushi Wakamatwa...
Wanajukwaa Poleni na Mahangaiko ya Duniani.
Jeshi la Polisi Tanzania kitengo cha Upelelezi limewakamata Vijana Watatu nchini Kenya. Vijana hao ambao walitoroka Mjini Zanzibar kwa Usafiri wa Mashua walinaswa wakiwa katika gari ndogo kutorokea Jijini Nairobi Nchini Kenya.
Mungu husimama Upande wa wenye Haki. Hii ni kwa mujibu wa Kipindi cha magazeti RFA. Nitawawekea habari kamili kutoka gazeti la Mtanzania muda mfupi ujao.
Watuhumiwa mauaji ya Padri Mushi wakamatwa
*Wadaiwa kusafiri kwa Jahazi kutoka Z’bar hadi Mombasa
*Wanaswa katika usafiri wa gari wakielekea mjini Nairobi
MAKACHERO wa Jeshi la Polisi nchini wamewatia mbaroni vijana watatu wanaotuhumiwa kuhusika katika mauaji ya Padri Everist Mushi (55) wa Kanisa Katoliki mjini Zanzibar.
Watuhumiwa hao wamekamatwa mjini Nairobi, Kenya kutokana na ushirikiano wa Jeshi la Polisi la Tanzania na Polisi wa Kenya kwa mwamvuli wa Shirikisho la Polisi wa Kimataifa (Interpol).
Habari za kuaminika kutoka Nairobi, Kenya zimesema kuwa watuhumiwa hao ambao majina yao yamehifadhiwa, walitiwa nguvuni juzi mjini humo walipowasili wakitokea Mombasa, mashariki mwa nchi hiyo.
Watuhumiwa hao ambao walikuwa wakiingia katika maficho kukwepa mkono wa dola, wanadaiwa kutumia jahazi kusafiria kutoka Zanzibar hadi Mombasa, Kenya kabla ya kusafiri kwa magari hadi Nairobi ambako walitiwa nguvuni.
“Tuliwakamata wakitokea Mombasa kwa basi kuja Nairobi. Baada ya kuwakamata tuliwafanyia mahojiano na baadaye tuliwakabidhi kwa polisi Tanzania,” kilisema chanzo chetu.
Tayari watuhumiwa hao ambao walikuwa wakifuatiliwa kwa karibu wamerejeshwa nchini kuunganishwa na watuhumiwa wengine waliopo katika mtandao huo.
Watuhumiwa hao walisafirishwa jana kwa magari kutoka Kenya kupitia mpakani Namanga wakiwa chini ya ulinzi mkali wa polisi.
Kukamatwa kwa watuhumiwa hao kunatokana na ushirikiano wa karibu wa majeshi ya polisi kwa ukanda wa nchi za Afrika Mashariki kwa mwamvuli wa Polisi wa Kimataifa (Interpol).
Watuhumiwa hao walitarajiwa kuwasili Dar es Salaam jana kabla ya kusafirishwa kwenda Zanzibar kuunganishwa na wenzao wengine kujibu tuhuma za mauaji zinazowakabili.
Alipotakiwa kutoa ufafanuzi kuhusiana na kukamatwa kwa watuhumiwa hao, Kamishna wa Polisi Zanzibar, Mussa Ali alisema hana taarifa zozote za kukamatwa kwa watuhumiwa waliohusika na mauaji ya Padri Mushi huko Kenya.
“Mimi sina taarifa zozote kama kuna watu waliokamatwa Kenya ambao wanahusishwa na mauaji ya Padri Mushi, lakini juhudi zetu za uchunguzi zinaendelea.
“Ninanchofahamu mimi ni kwamba wapo watuhumiwa ambao tunaendelea kuwahoji juu ya mauaji haya lakini sina taarifa za kukamatwa kwa watuhumiwa wengine nchini Kenya,” alisema.
Alipoulizwa iwapo kuna taarifa zozote ambazo zimefikishwa Interpol kwa msaada zaidi, Kamishna Mussa alisema: “Suala la wahalifu kuvuka mipaka inawezekana siwezi kukataa maana hawa ni binadamu.
“Lakini kuamini kuwa wanaweza kuvuka mipaka ni suala moja na suala la pili ni uchunguzi… Polisi haifanyi kazi kwa hisia tu tunajiridhisha kwa kufanya uchunguzi,” alisema.
Wakati huo huo, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein jana aliongoza mamia ya wananchi katika mazishi ya Padri Evarist Mushi katika eneo la Kitope, Wilaya ya Kaskazini B, Mkoa wa Kaskazini Unguja.
Mazishi hayo yalihudhuriwa na watu mbalimbali wakiwamo viongozi wa dini, mabalozi , wawakilishi, wabunge na viongozi wa vyama vya siasa kutoka Zanzibar na Tanzania Bara.
Mapema asubuhi jana, Dk. Shein alitoa salamu za mwisho kwa Padri Mushi huko katika kanisa la Minaramiwili mjini Zanzibar.
Sala ya mazishi kanisani hapo iliongozwa na Askofu Mkuu wa Kanisa Katoliki nchini, Muadhama Polycarp Kadinali Pengo na ibada ya mazishi huko Kitope iliongozwa na Mhashamu Baba Askofu Antoni Banzi ambaye ni Askofu wa Jimbo Katoliki Tanga.
Akitoa salamu za Serikali katika mazishi hayo, Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais Mohammed Aboud alisema Serikali imesikitishwa na kifo cha kiongozi huyo wa dini na kwamba ni huo ni msiba mkubwa kwa taifa.
Waziri Aboud aliwaomba wanafamilia wa marehemu na waumini wa dini ya Kikiristo kuwa watulivu na wastahamilivu katika kipindi hichi kigumu cha maombolezo ya kiongozi huyo.
Alimuelezea Padri Mushi kuwa alikuwa kiongozi aliyehubiri upendo, umoja na amani miongoni mwa waumini na wananchi wote wa Zanzibar na kuhimiza maadili mema hivyo kumuenzi kwa kumuombea maisha mema ya milele.
Nazo salamu za familia zilitolewa na Fransis Mushi na kutoa shukurani kwa niaba ya familia kwa ushirikiano mkubwa waliyoyapata katika msiba huo tokea siku ya tukio la mauaji ya Padri huyo hadi jana alipolazwa katika nyumba yake ya milele.
Naye Askofu Mkuu wa Kanisa Katoliki Zanzibar Augostino Shao alieleza kusikitishwa na msiba huo na kumuomea marehemu amani ya milele.
Padri Mushi alizaliwa Juni 15, 1957 katika kijiji cha Uru Kimanganuni katika Mkoa wa Kilimanjaro na baada ya kumaliza elimu ya juu ya Sekondari mwaka 1976, alijiunga na Seminari Kuu Kibosho ambako alipata elimu ya Falsafa kati ya mwaka 1978 na 1979.
Mwaka 1980 alijiunga na Seminari Kuu ya Mtakatifu Paulo, Kipalapala mkoani Tabora alipopata elimu ya dini (Theology) hadi mwaka 1982.
Mwaka 1984 alirudi Kipalapala mkoani Tabora kuendelea na masomo na mwaka huo huo alipata Daraja la Ushemasi katika Parokia ya Bikira Maria wa Rosari Kitope Zanzibar.
Katika maisha yake ya Upadri alishika vyeo mbalimbali ikiwamo Paroko wa Parokia ya Bikira Maria wa Rozari Kitope mwaka 1985, Paroko wa Parokia ya Moyo safi wa Maria wa Wete Pemba na Paroko wa Parokia ya Mtakatifu Antoni wa Padua Machui.
Padri Mushi aliuawa kwa kupigwa risasi Februari 17 Mtoni nje kidogo ya mji wa Zanzibar, na watu wasiojulikana.
No comments:
Post a Comment