Mzee Nelson Mandela ameendelea kuwa katika hali mbaya hospitalini jana baada ya kubainika kwamba gari la wagonjwa lililombeba Rais huyo wa zamani wa Afrika Kusini kwenda hospitali limeharibika.
Gari hilo la wagonjwa mahututi liliharibika wiki mbili zilizopita wakati Mandela alipokuwa akikimbizwa kwenye hospitali moja mjini Pretoria, na kumwacha 'njiapanda' kwa dakika 40.
Rais huyo wa zamani wa Afrika Kusini alihamishiwa kwenye gari jingine la wagonjwa la hospitali ya kijeshi kumalizia safari iliyobaki ya dakika 50 kati ya Johannesburg na Hospitali ya Moyo ya Medi-Clinic.
Msemaji wa Rais Mac Maharaj alisema: "Tahadhari zote zimechukuliwa kuhakikisha kwamba hali ya kiafya ya rais wa zamani Mandela haiathiriki na tukio hilo."
Madaktari wanaomtibu Mandela waliridhika kwamba hakupata maumivu yoyote katika kipindi hiki, aliongeza Maharaj.
Taarifa ya jana kuhusu afya ya Mandela inaonesha kwamba kuna mabadiliko kidogo katika hali ya shujaa huyo wa kupinga ubaguzi wa rangi tangu alipopokelewa hospitalini hapo.
Mandela, ambaye alikuwa rais wa kwanza mweusi wa Afrika Kusini mwaka 1994, alikimbizwa hospitali moja ya Pretoria mapema Juni 8 kufuatia maambukizi kwenye mapafu.
Ilidaiwa jana kwamba Mandela hajitingishi na familia yake sasa inajadili uwezekano wa kusitisha matibabu.
Amekuwa hospitalini kwa wiki mbili akipambana na maambukizi hayo, lakini taarifa zilizopita zimeashiria kwamba afya ya Mandela inaimarika.
Kwa mujibu wa vyanzo vipya, ufanyaji kazi wa ini na figo za Mandela umeshuka hadi asilimia 50 na hakufungua macho yake kwa siku kadhaa.
Pia alitakiwa kufanyiwa oparesheni mbili hivi karibuni, moja kutibu vidomda vya tumbo zilivyokuwa vikichuruzika damu na nyingine kuchomeka mpira mwilini mwake, imeripotiwa.
Taarifa hizi zinaashiria kwamba suala la Mandela ni kubwa kuliko inavyoripotiwa na mamlaka za Afrika Kusini.
Taarifa hizi zinaashiria kwamba suala la Mandela ni kubwa kuliko inavyoripotiwa na mamlaka za Afrika Kusini.
Historia ya matatizo ya mapafu ya Mandela ilianzia tangu alipokuwa kwenye gereza la Kisiwa cha Robben karibu na Cape Town. Aliachiwa huru mwaka 1990 baada ya miaka 27 na akaendelea kutumikia nchi kama Rais kuanzia mwaka 1994 hadi 1999.
Kulazwa kwake hospitalini ni mara ya nne tangu Desemba, mwaka jana.
No comments:
Post a Comment