Dar es Salaam. Waziri wa Mambo ya
Ndani ya Nchi, Dk Emmanuel Nchimbi jana alikuwa na wakati mgumu katika Kongamano
la Amani lililoandaliwa na Jumuiya ya Wanataaluma wa Chuo Kikuu cha Dar es
Salaam (Udasa), baada ya Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willbroad Slaa kumtaka
ajiuzulu kutokana na kushindwa kudhibiti uhalifu nchini.
Mbali ya Dk Nchimbi, Mwakilishi wa Mkuu wa
Majeshi katika kongamano hilo, Brigedia Jenerali, Elias Athanas naye alibanwa
akitakiwa kueleza tuhuma za askari wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ),
kuhusishwa na vitendo vya ubakaji na utesaji wa raia mjini
Mtwara.
Akizungumza katika kongamano hilo, Dk Slaa
alisema hakuna haja ya kutafuta mchawi wa amani ya nchi bali, Serikali inapaswa
kulaumiwa kutokana na watendaji wake kushindwa kuwajibika
ipasavyo.
Alitoa mfano wa kitendo cha Bandari ya Dar
es Salaam kutumiwa kupitisha pembe za ndovu wakati maofisa polisi wakiwemo ni
kitendo cha aibu ambacho kinatosha kumfanya Waziri Nchimbi
ajiuzulu.
Akijibu madai hayo wakati akihitimisha
kongamano hilo, Waziri Nchimbi alikiri kuwa baadhi ya polisi wamekuwa na tabia
ya kujihusisha na rushwa na katika kupambana na hali hiyo, Serikali imeshawatimu
kazi askari 101 katika kipindi cha mwaka 2012.
Hata hivyo, Dk Nchimbi alisema suluhisho la
matatizo yaliyopo ndani ya Jeshi la Polisi siyo kuwatimua kazi askari pekee na
ndiyo maana Serikali imeanza mkakati wa kutoa mafunzo ya maadili ili kuwawezesha
kufanya kazi zao kwa weledi.
Alisema ataendelea kupokea changamoto kutoka
kwa wadau wote wa amani na kupongeza waliobuni kongamano hilo, huku akiahidi
kutoa ushirikiano kufanikisha jambo lolote linalohusiana na mjadala wa amani ya
nchi.
Kuhusu ubakaji na utesaji wa wanajeshi, Dk
Slaa alisema inasikitisha kuona jeshi ambalo linapaswa kulinda amani linatesa na
kuwabaka raia.
Kauli hiyo iliungwa mkono na Naibu Katibu
Mkuu wa CUF, Julius Mtatiro ambaye alisema anao ushahidi wa wanachama wa chama
chake waliojeruhiwa na kupakwa pilipili akisema kwamba jeshi hilo limekuwa na
baadhi ya askari wakatili tofauti na misingi ya kuanzishwa
kwake.
Akijibu tuhuma hizo, Brigedia Jenerali
Athanas alikanusha madai hayo akisema siyo kweli kwamba JWTZ linaendesha unyama
na kwamba lipo Mtwara kwa ajili ya kulinda amani na kusema tuhuma hizo ni za
mitaani.
Mbunge wa Singida Mashariki (Chadema),
alidai kuwa tangu nchi ilipopata uhuru haijawahi kuwa na amani ya kweli akitoa
mfano wa wananchi kuhamishwa kwa nguvu katika maeneo yao.
Alisema katika siku za karibuni, tofauti na
zamani polisi ilipokuwa ikifanya kazi ya kudhibiti uhalifu, sasa inaonekana kama
kazi yake ni kudhibiti upinzani na limekuwa likituhumiwa mara kwa mara kwa
kufanya vitendo vya uvunjifu wa amani na kusababisha mauaji.
Alipiga kijembe akisema kwamba CCM
kinakaribia kuanguka na ndiyo maana kimekuwa kikitumia mabavu kudhibiti
upinzani.
Awali, Profesa wa Chuo Kikuu cha Dar es
Salaam, Gaudence Mpangala alisema amani inaweza kutoweka ikiwa CCM kitaendelea
kutumia dola kudhibiti upinzani.
Alisema CCM kinapaswa kufanya kazi kama
ilivyo vyama vingine vya siasa na kuonya kwamba hata kukiwa na makongamano
mengi, amani haitapatikana kama hakitajitathmini na kuchukua hatua.
Alisema polisi imekuwa ikifanya makosa
kuzuia maandamano ya vyama vya upinzani akisema sheria iko wazi ikisema
vinachotakiwa kufanya ni kulitaarifu jeshi hilo kuhusu ratiba ya shughuli
zake.
No comments:
Post a Comment