Hata katika uhusiano na mapenzi ni hivyohivyo. Kama hutakuwa mkweli, hutaishi maisha safi na utaonesha picha mbaya kwa jamii, kesho utakutana na majibu yake.
Umakini katika maisha ya uhusiano ni mzuri, kwanza kutakujenga kiakili, moyo hautakuwa na ukakasi maana una msimamo thabiti. Suala la kupenda ni muhimu.
Unaweza kupendwa lakini usipende. Unaweza kuwa na mwenzi wako ambaye mmefunga ndoa kabisa, lakini usiwe na mapenzi naye au pendo likapungua na baadaye kuyeyuka kabisa.
Hifadhi pendo moyoni mwako. Penzi ni uwekezaji. Lazima uwekeze pendo moyoni mwako, ujifunze kuwa katika uhusiano sahihi ili siku zijazo uyafurihie maisha.
Mapenzi hayatakuwa na maana kwako kama huna uwezo wa kupenda. Faragha haitakuwa na maana kwako kama hutakuwa na hamu na tendo lenyewe. Wengi wana tatizo hili lakini hawajajua namna ya kujitibu.
Wengi huona ufahari kuwa na wenzi wengi lakini athari zake kisaikolojia ni kubwa. Mahodari wa wenzi wengi hupoteza uwezo wa kupenda na hamu ya tendo.
Hujawahi kuona baba/mama mtu mzima kabisa, mweye miaka zaidi ya 50 bado anafukuzana na dogodogo? Unadhani anatafuta nini alichokosa kwa mwenzake? Si kweli kwamba mwenzake hana uwezo kama zamani.
Ni athari ya kutotosheka. Kama mtu umempenda, hata akizeeka, mnazeeka pamoja. Mnalandana kwa kila kitu kwahiyo hata mapenzi nayo huongezeka zaidi. Kuona watu wazima wakikimbizana na watoto huko nje, maana yake ni wagonjwa! Wameshaathiriwa na mfumo mbaya huko nyuma.
TAFITI MWENYEWE
Fanya uchunguzi mdogo utagundua kuwa, hata hao watu wazima wenye wapenzi ‘dogodogo’ huwa hawawezi kuwa na mmoja tu. Leo huyu, kesho yule! Ni kwa sababu anaumwa na anajaribu kutafuta tiba ambayo si sahihi kwa hakika.
Tiba yake ni ushauri tu. Akalishwe chini na kuelezwa anapokosea ni wapi na kumtengeneza ‘mtu’ mwingine kichwani mwake.
USHAHIDI
Utafiti unaonyesha kuwa, mtu aliyepata kuwa katika uhusiano na wenzi wengi hupoteza uwezo wa kupenda. Yaani anakuwa na mtu leo akiamini kuwa amempenda lakini akishakutana naye faragha anajikuta hamu ya kuwa naye imetoweka!
Wengi kuanzia hapo wanaanza kuwachukia. Tabia hiyo huota mizizi na kujikuta kila wakati akiingia katika uhusiano mpya.
LADHA HUONDOKA
Aidha, mtu ambaye amezoea kukutana na mapatna wengi, hupoteza hamu au kukosa ladha ya tendo. Watu wa namna hii, hujikuta wakiwajua watu wa jinsi pacha ‘sana’ kiasi cha kuanza kuwa wakaguzi mno na mwishowe hamu au ladha hupungua kama siyo kupotea kabisa.
Mariam (si jina halisi) mkazi wa Sinza, Dar ni mwanandoa. Ana miaka 34. Ana watoto wawili na mumewe ambaye ni mwajiriwa serikalini. Alifika ofisini wikiendi iliyopita kunitaka ushauri.
Alisema: “Mume wangu amenizidi umri kidogo, yeye ana miaka 44. Anatunza familia yake vizuri. Mimi na watoto tunaishi vizuri lakini tatizo huyu bwana ni mhuni sana. Yaani asione mwanamke mbele yake. Kishatembea na mahausigeli zaidi ya wanne, nikaamua kumleta ndugu yangu, naye akalala naye.
“Ni mwanaume nisiyemwelewa kabisa. Hilo linanifanya nikose amani na ndoa yangu, maana hata faragha anakuwa goigoi. Anajijali mwenyewe, yaani ndoa naiona chungu.”
Baada ya mazungumzo marefu na kumwuliza vizuri kuhusu historia yao ya uhusiano, ilionyesha kwamba mumewe ana tatizo hilo la kupoteza uwezo wa kupenda na kukosa hamu ya tendo. Nilimaliza kesi yake vizuri.
Inawezekana nawe una tatizo kama hilo lakini hujui namna ya kujiondoa, kesho tutakuletea sehemu ya pili ya mada yetu ya namna ya kumvutia yule aliyeuteka moyo wako, USIKOSE!
No comments:
Post a Comment