WATU watatu wa familia moja wamefariki dunia baada ya pikipiki waliyokuwa wamepanda kugongwa na basi la Kampuni ya Mtei Express katika Kijiji cha Kisasida, nje kidogo ya Manispaa ya Singida.
Ajali hiyo ilihusisha pikipiki T 368 BXZ Skygo na basi T 742 ACU Scania lililokuwa linatoka Singida kwenda Arusha.
Waliokufa katika ajali hiyo ambao walikuwa wakienda shambani ni Stamili Shaban na Kasim Shaban waliofariki dunia eneo la tukio na Hamza Shaban akifia katika Hospitali ya Mkoa wa Singida.
Kwa mujibu wa mashuhuda, mwendesha pikipiki, Shaban Bunku, aliyekuwa amepakia abiria watatu, alilipita basi hilo kisha kukata kona, hali iliyosababisha kugongwa kwa nyuma na basi hilo.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Singida, Geofrey Kamwela, aliyefika eneo la tukio, alithibitisha kutokea kwa ajali hiyo na kusema baada ya ajali wananchi walilichoma moto basi hilo.
Hata hivyo alisema gari la zimamoto lilifika na kufanikiwa kulizima kabla ya kuteketea kabisa.
Kamanda Kamwela aliwaaasa wananchi kuacha kujichukulia sheria mikononi ajali zinapotokea, badala yake watii sheria.
Alisema dereva wa basi hilo, Dismas Ludovick, mkazi wa Singida alikimbia baada ya ajali hiyo.
Source Tanzania Daima
No comments:
Post a Comment