Saturday, September 14

Serikali yakata mawasiliano na WAPINZANI...Yaapa kutowaalika tena IKULU


 
WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais (Uhusiano na Uratibu), Steven Wassira, amesema wapinzani wasitarajie tena kukaribishwa Ikulu, kutokana na msimamo wao wa kususia mjadala wa Muswada wa Marekebisho ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba wa mwaka 2013, wakati wa kikao cha Bunge mjini Dodoma hivi karibuni, kwa majadiliano mengine.

Waziri Wassira, alitoa kauli hiyo siku moja baada ya wasomi, wanasiasa na wanaharakati kutoa ushauri wa kumsihi Rais Jakaya Kikwete asisaini muswada huo ili kuwa sheria kamili, kwa vile hauna tija kwa Watanzania.

Akizungumza na MTANZANIA jana juu ya ushauri huo, Wassira alisema hoja na ushauri unaotolewa na makundi hayo hauna mantiki kwa sababu taratibu zote za sheria zilifuatwa, kuanzia mwanzo hadi kuupitisha muswada huo.

“Nianze kwa wanasiasa wa upinzani kususia na kutoka ndani ya Bunge kwa hoja ya kutowashirikisha wananchi wa Zanzibar, hili si kweli, kwa sababu Kamati ya Katiba na Sheria ilikwenda huko, sasa wasitake kulalamika na kutaka kukutana na Rais Kikwete.

“Hawa tumewalea siku nyingi na sasa wanafanya mazoea, ninachotaka kuwaeleza wasitarajie tena kuitwa Ikulu, nchi hii inaongozwa na misingi na kufuata taratibu zilizowekwa kwa mujibu wa sheria.

“Kwanza kitendo cha Kiongozi wa Upinzani, Freeman Mbowe kutotii kiti cha Spika wa Bunge ni dharau na alikiuka taratibu zinazoongoza Bunge, kwanza alisababisha kuwapo vurumai ambazo zimeshusha heshima ya Bunge.

“Upinzani wajue vurumai zao haziwezi kutengeneza Katiba wanayoitaka Watanzania, bali ni kufuata taratibu pale wanapoona kuna kasoro, hivyo kulalamika kwao bila kufuata taratibu hakutawasaidia kamwe.

“Kuna mazoea ya kwenda kwa wananchi kuwadanganya, sasa tunasubiri tumesikia wanaandaa tamko lao la upinzani, tutalisoma na kama wakienda kwa wananchi kueneza propaganda zao tutawafuata nyuma na kuwaeleza ukweli wananchi,” alisema.

Alisema Watanzania milioni 45, hawawezi kuaminishwa uongo wakati Serikali ipo na kuongeza kwamba nchi haiwezi kuendeshwa na vurugu wakati kuna vyombo vya dola vyenye mamlaka yake.

Kuhusu ushauri wa wasomi kutaka Rais Kikwete kukutana na wanaolalamika, alisema inategemea na utashi wake na jinsi atakavyoona inafaa.

Alisema imegundulika wasomi wa vyuo vikuu mbalimbali wamekuwa wakitumia mwavuli wa elimu yao kutoa maoni yao ambayo yanaonekana wazi ni ya itikadi ya vyama vya siasa.

“Hawa wanaojiita wasomi wote wana itikadi ya vyama vya siasa, sasa badala ya kutoa ushauri ambao utaonekana ni wa msomi, wanajikuta wanakuwa sehemu ya siasa tena.

“Sasa watu kama hao inapaswa kuwaangalia kwa makini sana, kwa sababu wanafanya kazi ya chama cha siasa kwa kutumia mwavuli wa usomi wake, hivyo hivyo kwa wanaharakati, badala ya kufanya kazi kama ilivyoelekezwa kwenye usajili wao, nao wanaingia kwenye siasa.

“Ninachowashauri, nchi hii haiendeshwi kwa ubabe, bali inasimamiwa na sheria, hivyo kila mmoja akifuata sheria hakuna ugomvi, pia haya madai ya kusema kuwa Katiba ijayo itakuwa ni ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) hayana msingi wowote,” alisema.

Juzi wasomi kutoka vyuo mbalimbali, kikiwamo Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Chuo Kikuu cha Tunguu kilichopo Zanzibar na vingine, walitoa ushauri wao wa kumtaka Rais Kikwete kufikiri zaidi na kuchukua tahadhari kabla ya kusaini muswada huo ili kuwa sheria kamili.

Katika hatua nyingine, Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Katiba na Sheria, Pindi Chana, alipoulizwa na MTANZANIA kuhusiana na malalamiko hayo, alisema: “Kamati yangu ilifanya kazi iliyotumwa na taratibu zote zilifuatwa.”

No comments:

Post a Comment

Search This Blog