Hakuna anayependa kupata maradhi ya zinaa, lakini kama kwa bahati mbaya utapata ugonjwa kama Gonorea au Pangusa, magonjwa ambayo awali yalionekana kama yanayotibika kirahisi, hivi sasa wataalamu wa tiba huko kwa wenzetu wamethibitisha kwamba, maradhi hayo huenda ikawa ngumu kutibika kama ilivyodhaniwa.

Utafiti uliofanywa hivi karibuni huko nchini Marekani umebaini kwamba zile dawa zilizokuwa zikiaminiwa kwamba zinatibu magonjwa ya zinaa kama hayo niliyoyataja zimeonekana kushindwa kukabiliana na magonjwa hayo. Kwa mujibu wa wataalamu hao walisema kwamba huu ni wakati wa kuchukua tahadhari kabla ya hatari.

“Tishio hili sio la kubeza, kwani Gonorea ni gonjwa la pili linaloongoza nchini Marekani” Walisema wataalamu hao. Inadaiwa kwamba takriban watu 600,000 waliripotiwa kuugua ugonjwa huo kwa mwaka nchini Marekani na mojawapo ya athari walizopata watu waliougua ugonjwa huo ni matatizo katika mfumo wa uzazi, na kwa upande wa wanawake wataalamu hao walieleza kwamba, wanaweza kuwaambukiza watoto wao wakati wa kujifungua.

“Ni vyema hivi sasa watu wakachukua tahadhari ili kuepuka magonjwa hayo ya zinaa, kwani athari zake ni kubwa kuliko inavyodhaniwa” walisema wataalamu hao………….

Haya sasa, wale waliokuwa wakiona kuwa Ukimwi ni tishio, kimbembe kingine hiki hapa.