MWENYEKITI wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Freeman Mbowe, Mbunge wa Sengerema (CCM), William Ngeleja na Mfanyabiashara maarufu, Rostam Aziz, wamehojiwa kuhusu kuwa na utajiri mkubwa nje ya nchi.
Wanasiasa hao wamehojiwa na kikosi kazi maalumu kilichoundwa na serikali hivi karibuni kwa ajili ya kutafuta mali mbalimbali zilizofichwa nje ya nchi na watu mbalimbai wenye nyadhifa kubwa.
Ingawa watendaji wakuu wa kikosi kazi hicho wamekataa kuthibitisha au kukana kuhusu kuhojiwa kwa wanasiasa hao, Raia Mwema limeambiwa wanasiasa hao ni sehemu tu ya watu zaidi ya 100 wanaochunguzwa na vyombo vya dola.
Kikosi hicho kiliundwa na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda na kinaongozwa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Jaji Frederick Werema, Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Dk. Edward Hoseah na wawakilishi kutoka Jeshi la Polisi, Benki Kuu ya Tanzania (BoT) na waatalamu wa masuala ya kibenki.
Chanzo cha kuaminika cha kilisema Mbowe ambaye pia ndiye Kiongozi wa Upinzani Bungeni, alihojiwa kutokana na maelezo kuwa alinunua jumba la kifahari nchini Dubai, Desemba mwaka 2011.
“Kutokana na wadhifa wake kwa umma, Mbowe ilibidi achunguzwe kutokana na ununuzi wa nyumba alioufanya nchini Dubai, Desemba mwaka 2011.
Uchunguzi wake ni mahususi kwa sababu tumefuatilia akaunti zake na ikaonekana hakuwahi kutumia njia ya benki kufanya malipo.
“Hii maana yake ni kwamba kama alifanya malipo, basi alifanya kwa kutumia fedha taslim (cash).
Sasa ni lazima ichunguzwe maana si kawaida kwa kiongozi kama yeye kusafiri na mamilioni yote ya kununua jumba kule Dubai na kulipa cash. Ndiyo maana yeye anafanyiwa uchunguzi mahususi,” kilisema chanzo cha kuaminika cha gazeti hili.
Rostam ni miongoni mwa wafanyabiashara maarufu hapa nchini na Raia Mwema limeelezwa kwamba alihojiwa kutokana na kumiliki jumba katika nchi hiyo ya Mashariki ya Kati na imeelezwa pia kuwa ana akaunti kadhaa nje ya nchi.
Dubai ni kimbilio la wafanyabiashara wengi kutokana na nafuu ya kodi inayotolewa na serikali ya nchi hiyo na pia uwepo wa biashara na usalama mkubwa uliopo.
Zaidi ya kuwa mfanyabiashara maarufu, Rostam aliwahi kuwa mbunge kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) na alipata pia kuwa Mweka Hazina wa chama hicho.
Hadi tunakwenda mitamboni, gazeti hili lilikuwa halijafahamu ni kwa sababu ya mali zipi hasa ambazo Ngeleja anazo lakini wakati akiwa Waziri wa Nishati na Madini, kulikuwa na minong’ono kwamba alikuwa miongoni mwa mawaziri vijana wenye ukwasi mkubwa alioukwaa ndani ya muda mfupi.
Alipoulizwa na Raia Mwema kuhusu alichohojiwa alipoitwa na kikosi kazi, Ngeleja alijibu kwa ujumbe mfupi wa maneno kupitia simu yake ya mkononi; “Samahani, mimi si msemaji wa suala hilo.” Hata alipoombwa na mwandishi walau kukanusha au kukataa kuwa alihojiwa – Ngeleja alijibu kwa ufupi, “Ahsante.”
Kwa sasa, waziri huyo wa zamani wa serikali ya Rais Jakaya Kikwete yuko safarini nje ya nchi.
Alipotafutwa wiki hii kueleza upande wake kuhusu alichohojiwa, Rostam hakujibu simu wala ujumbe mfupi wa maneno aliotumiwa na mwandishi.
Mbowe hakuwa tayari kueleza kuhusu kuhojiwa huko ingawa Ofisa Habari wa CHADEMA, Tumaini Makene, aliyeeleza kuwa ameagizwa kujibu kwa niaba ya mkuu huyo wa upinzani, alisema; “si jambo la ajabu kwa Mbowe kuwa na mali nje ya nchi kwa vile ni mfanyabiashara na ana biashara hadi nje ya nchi.”
Kikosi kazi kinafanya kazi zake katika mazingira ya usiri na tangu kilipoanza kazi mapema mwaka huu, hakijawahi kutoa taarifa rasmi kuhusu shughuli zake.
Mmoja wa wajumbe wa kikosi kazi hicho, Dk. Hoseah alikataa kuzungumza chochote kuhusu watu waliowahoji kwa maelezo kuwa msemaji wa shughuli yao ni Werema.
Werema hakutaka kukana wala kuthibitisha taarifa hii isipokuwa katika mazungumzo ya nyuma na vyombo vya habari aliwahi kusema kwamba ni kinyume cha maadili kwa tume hiyo kutoa taarifa kuhusu watu iliowahoji.
Raia Mwema linafahamu kwamba mtu kuhojiwa na kikosi hicho haimaanishi moja kwa moja kwamba ni fisadi isipokuwa mahojiano yanafanyika kwa minajili ya kukusanya taarifa.
Novemba mwaka jana, Mbunge wa Kigoma Kaskazini (CHADEMA), Zitto Kabwe, alitoa hoja binafsi bungeni akitaka ufanyike uchunguzi wa fedha na mali haramu kutoka Tanzania zilizofichwa katika nchimbalimbali duniani.
Kwa mujibu wa sheria za Tanzania, raia wake hawaruhusiwi kufungua akaunti katika nchi za kigeni pasipo ruhusa ya ofisi ya Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania.
Katika hoja yake binafsi, Zitto alitaka Bunge lipewe nguvu ya kuunda Kamati Teule ambayo itachunguza na kubaini ni akina nani wanamiliki akaunti na mali ughaibuni lakini serikali iliamua yenyewe kuwa ndiyo itafuatilia kwa kutumia vyombo vyake.
-Raia Mwema
No comments:
Post a Comment