Monday, October 21

UFOO SARO..."NIKIPONA NITAWEKA KILA KITU WAZI"


Mtangazaji wa Kituo cha televisheni cha ITV, Ufoo Saro, ambaye alijeruhiwa kwa kupigwa risasi na mzazi mwenzake Jumapili iliyopita, ameahidi kutoa ya moyoni atakapopona na kuruhusiwa kutoka hospitalini.Ufoo ambaye amelazwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, kitengo cha moyo tangu wiki iliyopita kutokana na majeraha ya risasi, afya yake inazidi kuimarika na sasa ameanza kula mwenyewe na kufanya mazoezi ya kutembea.


Ufoo kwa sasa haruhusiwi kuonwa au kuzungumza na watu ovyo kutokana na ushauri wa daktari wa kutaka apumzike kwa muda mrefu.Mtangazaji huyo alipigwa risasi mbili na mzazi mwenzake ambaye kwa sasa ni marehemu, Anthery Mushi, katika ugomvi unaodaiwa kuwa ni wa kifamilia ambapo mama yake mzazi Ufoo, Anastazia Saro aliuawa.

Akizungumza na waandishi wa habari jana katika wodi ya moyo, Saro, ambaye alikutwa na mwandishi wetu akiwa amekaa kwenye kiti, alisema anamshukuru Mungu kutokana na matibabu ya takribani wiki moja yaliyomwezesha kuanza kula chakula laini na kufanya mazoezi ya kutembea na kukaa.

"Na mshukuru sana Mungu, kwani sikutegemea kama mimi nitapona kutokana na kupata majeraha makubwa katika mwili wangu, kwani nilijua nitaiaga dunia,'' alisema.

Aliongeza kuwa, anawashukuru watu wote waliofanikisha kupatiwa matibabu hayo, na hali hiyo imesaidia afya yake hivi sasa kuzidi kuimarika.

Alipoulizwa kuhusu chanzo cha tukio hilo, Ufoo alisema kuwa hayupo tayari kulizungumzia suala hilo kwa sasa, lakini aliahidi kuzungumza siku ambayo atakuwa amepona kabisa na umma utajua ni nini kilitokea.

"Siwezi kusema kitu chochote sasa hivi ngoja nipone kabisa kila kitu nitakiweka wazi,'' alisema.

Naye dada wa Ufoo Julieth Saro, ambaye analala na Ufoo katika wodi hiyo, aliiambia NIPASHE kuwa hali yake (Ufoo) inazidi kuimarika kila siku kutokana na matibabu anayopata kutoka kwa madaktari wake.

"Tunamshukuru sana Mungu kwa kumuwezesha kupata matibabu ambayo yamesaidia hali yake kuzidi kuimarika kila siku na kuzidi kutupa matumaini sisi wanafamilia,'' alisema.

Afisa uhusiano wa Muhimbili, Aminiel Aligaesha, aliiambia NIPASHE kuwa hali ya Ufoo inaendelea vizuri kutokana na juhudi ambazo zimekuwa zikifanywa na madaktari bingwa wa kitengo cha moyo.

Aliongeza kuwa Ufoo alipoletwa hapa hospitalini alikuwa ana hali mbaya na alikuwa hawezi kula wala kutembea, lakini baada ya kupatiwa matibabu hivi sasa anafanya mazoezi ya kutembea pamoja na kula chakula.

Alisema kuwa Ufoo anaweza kuruhusiwa muda wowote ule kutokana na hali yake kuendelea vizuri.

"Japo mimi siyo daktari wake wa kulizungumzia hilo ni lini ataruhusiwa, lakini anaweza kuruhusiwa muda wowote ule kutokana na hali yake kuwa nzuri, kwani hivi sasa anaweza kula na kutembea,'' alisema.

Oktoba 13, mwaka huu, majira ya saa 12.30 alfajiri, mzazi mwenziwe Ufoo, Mushi alimpiga risasi mama mkwe wake na kuumua, kumpiga risasi Ufoo na kisha kujiua mwenyewe

No comments:

Post a Comment

Search This Blog